1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTogo

Togo yapiga kura ya wabunge baada ya mageuzi ya kikatiba

Tatu Karema
30 Aprili 2024

Raia wa Togo wamepiga kura kuwachagua wabunge baada ya mageuzi ya kikatiba yaliyosababisha mgawanyiko ambao wapinzani wanasema yanampa Rais Faure Gnassingbe mwanya wa kuongeza muda wa kuendelea kushika madaraka

https://p.dw.com/p/4fKcK
Rais wa Togo  Faure Gnassingbe akiwa katika mkutano na Gerd Müller mjini Lome, Juni 14, 2021.
Rais wa Togo Faure GnassingbePicha: Ute Grabowsky/photothek/IMAGO

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa vituo vya kura vilifungwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni na baada ya hapo kura zikaanza kuhesabiwa. Taarifa ya tume ya uchaguzi nchini humo ilikuwa imesema kwamba huenda matokeo ya awali yangelianza kutolewa jana jioni.

Makamu wakuu wa mikoa 179 wachaguliwa 

Zoezi hilo ni la kuwachagua wabunge 113 na pia kwa mara ya kwanza, makamu wakuu wa mikoa 179 katika wilaya tano ambao pamoja na madiwani watachagua baraza jipya lililoundwa la seneti.

Kulingana na chama tawala chaGnassingbe, UNIR, hatua hiyo inaifanya Togo kuwa na uwakilishi zaidi lakini vyama vya upinzani viliwahamasisha wafuasi kupiga kura dhidi ya kile walichokitaja kuwa mapinduzi ya kitaasisi.

Soma pia:Kampeni zamalizika Togo kabla ya uchaguzi muhimu wa Jumatatu

Baada ya kupiga kura hapo jana, Jean- Pierre Fabre, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, National Alliance for Change, alisema walikuwa na kampeini nzuri ya uchaguzi na kwamba wanalaani kasoro za uongozi uliopo madarakani huku akiongeza kuwa raia wa Togo watafanya maamuzi bora.

Mpiga kura akipiga kura katika kituo cha shule ya msingi ya umma ya Hedzranawoe mjini Lome Aprili 29, 2024.
Raia wa Togo apiga kura ya kuwachagua wabungePicha: Emile Kouton/AFP

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, ilikuwa imesema kuwa itatuma timu ya waangalizi nchini Togo kufuatilia zoezi hilo la uchaguzi.

Wakati wa kupiga kura, tume ya uchaguzi nchini humo, ilikataa kuruhusu Baraza la Maaskofu wa nchi hiyo kupeleka waangalizi wa uchaguzi kote nchini humo.

Soma pia:Togo: Wabunge sasa kumchagua Rais katika katiba mpya

Kwa upande wake, shirika la kutetea haki la Amnesty International limetoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kukomesha ukandamizaji unaoongezeka.

Upinzani Togo haufurahii haki ya kujieleza

Mkurugenzi wa shirika hilo kwa Afrika Magharibi na Kati Samira Daoud, amesema nchini Togo,sauti za upinzani hazifurahii haki yao ya kujieleza na mikutano ya amani. Daoud ameongeza kuwa imekuwa vigumu kuchangia kwa njia huru kwenye mjadala kuhusu katiba mpya kutokana na uoga wa hatua za kisasi.

Wabunge waliidhinisha nafasi inayofanana na ya waziri mkuu

Kura hiyo imefanyika baada ya wabunge mwezi huu kupiga kura kuidhinisha kuwepo kwa nafasi inayofanana na ya waziri mkuu ambayo kulingana na wapinzani, iliundwa ili kumsaidia Rais Gnassingbe kuepukana na ukomo wa kukaa madarakani.

Tayari  Gnassingbe, mwenye umri wa miaka 57, ameshashinda katika chaguzi nne ambazo zote zilipingwa na vyama vya upinzani kutokana na kile walichokiita kuwa ni dosari. Kulingana na katiba ya awali, Gnassingbe angeweza kugombea urais mwaka 2025 pekee katika muhula mmoja uliosalia.